Naibu waziri wa ardhi ,nyumba na maendeleo ya makazi Mhe.Angelina Mabula ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa SIMIYU kutumia fursa za nyumba za makazi zinazotarajiwa kujengwa katika eneo la Isanga Mjini Bariadi na Shirika la Nyumba la Taifa
Wito huo ameutoa mkoani Simiyu alipokutana na wadau mbalimbali katika kongamano la ujenzi wa nyumba za makazi mkoani Simiyu lililohudhuriwa na viongozi wa serikali mkoani humo wakiongozwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa mkoa wa Simiyu,wakuu wa wilaya wakurugenzi, makatibu tawala wilaya, wakuu wa idara na watumishi wa kada mbalimbali kutoka halmashauri zote, wafanyabiashara na viongozi wa vyama vya wafanyakazi lengo likiwa ni kuangalia aina ya nyumba zitakazojengwa na Wateja watarajiwa.
Mabula amesema azma ya wizara ya ardhi ,nyumba na maendeleo ya makazi ni kumwezesha kila mtanzania kunufaika na nyumba zinazojengwa na shirika hilo, huku akisisitiza Taasisi nyingine zinazohusika na uwekaji wa miundombinu muhimu kuanza utaratibu wa kuweka miundombinu hiyo ili kuwapunguzia gharama wanunuzi.
“ Tunatarajia taasisi zinazohusika ziwe zimeshaanza kupeleka huduma huko, wakati NHC wanaanza kujenga nyumba zao pale gharama itakuwa iko chini kwa sababu hivi vitu vingine vitakuwa vimewekwa na taasisi nyingine na kazi yao itakuwa ni kurudiisha fedha zao kupitia bili za umeme, maji”
“Awali nyumba za NHC zilikuwa zikilalamikiwa kuwa ni za gharama kubwa kutokana na wao kufanya kazi zote wao wenyewe, ujenzi wa nyumba na uwekaji wa miundombinu ya maji , umeme, barabara, viwanja vya michezo na huduma nyingine, lakini tunamshukuru Mhe. Rais alishatoa maelekezo kwa wizara na mamlaka husika kuhakikisha wanaweka miundombinu ya huduma zote muhimu mahali ambapo NHC wanajenga nyumba zao” alisema.
Wakitoa maoni yao baadhi ya wadau wametoa ushauri kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuona namna ya kujenga nyumba zenye gharama nafuu zaidi ili wananchi wengi hususani wale wenye kipato cha chini waweze kunufaika na mradi huu.
“Ninaiomba Serikali kuangalia upya gharama za nyumba za makazi zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa(NHC) ili kuwawezesha watumishi na wananchi wengi kumudu gharama za kununua nyumba hizo kwa kuwa wengi ni wenye vipato vya chini, pia benki zinazowakopesha wananchi wanaonunua nyumba hizo zitoe mikopo kwa masharti ambayo hayatawaumiza wakopaji” alisema Mbunge wa Itilima, Mhe. Njalu Silanga.
“Ninashauri Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuona haja ya kuwa na mpango mkakati wa kuboresha makazi ya wakulima ambao wamejiunga na Vyama vya Ushirika vya Msingi(AMCOS) ili vyama hivyo, benki pamoja na NHC waje namna kujenga nyumba zenye bei nafuu zaidi na kundi kubwa zaidi liweze kunufaika” alisema Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Dkt. Fredrick Sagamiko.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa kuwa chachu ya Maendeleo ya makazi bora nchini, huku akibainisha kuwa Shirika hilo linaweza kuona namna ya kufanya kazi na Halmashauri mkoani humo katika kukabiliana na changamoto ya makazi kwa watumishi.
Wakizungumza katika Kongamano hilo Wawakilishi wa taasisi za fedha zikiwemo Benki za NMB, CRDB na Azania Bank wamesema wamejipanga katika utoaji wa mikopo ya nyumba kwa wale walio tayari na wenye vigezo vinavyotakiwa.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/10/naibu-waziri-mabula-atoa-wito-wananchi.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa