Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amemuagiza Mrajisi msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Simiyu, Bw. Ibrahim Kadudu kutoa vibali kwa wafanyabiashara wa choroko kwa ajili ya kusafirisha maeneo mbalimbali mara bada ya kulipa ushuru wa Halmashauri na Vyama vya msingi vya Ushirika (AMCOS).
Agizo hilo lilitolewa jana na kuwasilishwa kwa niaba yake na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi.Miriam Mmbaga wakati wa kuhitimisha kikao cha mkoa cha wadau wa zao la choroko kilichofanyika Machi 01, 2021 Mjini Bariadi kwa ajili ya kujadili utaratibu wa uuzaji choroko.
“Mrajisi unatakiwa utoe vibali vya kusafirisha choroko ambazo zipo tayari, na vibali hivyo vitolewe mara baada ya wafanyabiashara hao kulipa ushuru wa Halmashauri na AMCOS; ili kuepusha usumbufu ni vema tukaweka utaratibu ili kuhakikisha kuwa malipo yote yanafanyika Halmashauri,”
“Ili Mkulima na mfanyabishara waweze kunufaika na bidhaa za kilimo ni vyema kila mmoja wao akafuata taratibu, Kanuni na sheria zilizotolewa na Tume ya Ushirika, kwa msimu huu wa choroko ni vyema Choroko zote ziingie kwenye minada, hii Itamsaidia mkulima kupata bei shindani,” alisema.
Awali akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka alitoa wito kwa viongozi kulijadili suala la ununuzi wa Choroko na kufanya maamuzi kulingana na mazingira ya mkoa ili kulinda maslahi ya Serikali, Mkulima na Mfanyabiashara.
Aidha, Mtaka ameongeza kuwa badala ya wakulima kuwekewa vikwazo, ni vema ikaangaliwa namna ya kuwasaidia wakulima kwa kuwa zao la choroko limekuwa zao la pili la biashara, Mkoani Simiyu baada ya zao la pamba.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupitia mkoa wa Simiyu, Mhe. Gungu Silanga akichangia hoja katika kikao hicho ameshauri kuwa wakulima na wafanyabiashara wapewe elimu zaidi kuhusu mfumo wa stakabadhi ghalani waelewe ili utumike wakati mwingine lakini kwa sasa wakulima wapewe uhuru wa kuuza choroko zao kupitia mfumo huo au soko huria.
Aidha, amewasisitiza Wafanyabiashara kuhakikisha wanalipa ushuru na tozo zote wanazopaswa kulipakama inavyoelekezwa na Serikali.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa Wa Simiyu, Bw. John Sabu amesema ni vema Vyama vya Ushirika vitafute mtaji navyo viingie sokoni kununua choroko kama wafanyabiashara wengine na ili kumuepushia usumbufu Mfanyabiashara ni vyema Malipo yote ya ushuru yafanyike mahala pamoja.
Mbunge wa Kisesa, Mhe.Luhaga Mpina amesema Mwongozo wa stakabadhi ghalani umekuja wakati wakulima tayari wameshalima yaani baada ya biashara na tayari wafanyabiashara wameshaingia gharama hivyo lipewe muda na wakulima/ wafanya biashara waelimishwe.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bariadi, Mhe. Juliana Mahongo amependekeza kuwa Ushirika uangaliwe kwa nchi nzima,na upelekwe msaada bungeni ili kuhakikisha kwamba ushirika wetu unaimarishwa kwa manufaa ya wananchi na si kuwakandamiza watu.
Mrajisi Mkoa wa Simiyu Bw. Ibrahim Kadudu amesema Ilani ya Chama kuhusu ushirika ni kusogeza huduma kwa wananchi na kuboresha maisha ya wananchi na kusisitiza kuwa Mfumo wa stakabadhi ghalani ulianza mwaka 2020, na wakulima walikubali kwamba wataanza kutumia mfumo huo mwaka huu.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2021/03/mrajisi-atakiwa-kutoa-vibali-kwa.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa