Mkuu wa JKT nchini Meja Jenerali Charles Mbuge wamefanya ziara ya siku moja mkoani Simiyu kwa lengo la kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi hilo SUMA JKT.
Akikagua miradi hiyo jana Julai 03, 2020 Meja Jenerali Mbuge amewataka wasimamizi wa miradi hiyo kuongeza kasi katika utekeleza ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati.
“Nataka site (maeneo ya kazi) zichangamke, hakikisheni mnaongeza watenda kazi wakiwemo mafundi na vibarua; tafuteni mashine zenye uwezo wa kufyatua tofali nyingi kwa wakati mmoja ili kazi iende kwa kasi na viwango," alisema Mbuge.
Aidha, Brigedia Jenerali Mbuge amewaagiza viongozi wote wanaosimamia utekelezaji wa miradi hiyo kuhakikisha kuwa wanafanya kazi bila kusimamiwa huku akisisitiza kuwa atafuatilia utekelezaji wa maagizo yote aliyoyatoa kwa viongozi wa JKT ambao ni wasimamizi wa miradi hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema Serikali ya Mkoa inatambua kazi nzuri inayofanywa na SUMA JKT mkoani hapa, huku akibainisha kuwa anatarajia kuona matokeo zaidi baada ya ziara ya Mkuu wa JKT kutokana na maelekezo aliyotoa kwa wasaidizi wake ambayo mengine amehusika moja kwa moja kuwa sehemu kubwa ya utatuzi wa changamoto kwenye miradi hiyo.
"Ziara hii imekuwa ziara darasa na sisi kama viongozi tumejifunza mengi kwako Mkuu wa JKT hasa katika suala la kufanya maamuzi; tunategemea kuona matokeo baada ya ziara hii kutokana na maelekezo uliyoyatoa," alisema Mtaka.
Naye Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Donatus Weginah amesema Serikali ya Mkoa na taasisi za Umma zilizopo inaunga mkono SUMA JKT huku akiomba zaidi ya shilingi milioni 700 zilizolipwa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu zitumike kufanya kazi hiyo ili kutoa nafasi kwa Katibu Tawala Mkoa kupewa fedha nyingine na lengo la kukamilisha jengo hilo Desemba 2020 litimie.
Msimamizi Mkuu wa SUMA JKT Kanda ya Ziwa, Kapteni Fabian Buberwa ameahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa JKT na kusisitiza kuaysimamia kwa kadri alivyoelekeza.
SUMA JKT katika Mkoa wa Simiyu inatekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa , ujenzi wa jengo la wizara ya kilimo katika uwanja wa nanenane Nyakabindi, ujenzi wa kiwanda cha chaki na kiwanda cha vifungashio.
MWISHO.
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2020/07/mkuu-wa-jkt-afanya-ziara-simiyu-kukagua.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa