Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade ) Edwin Rutageruka ametoa wito kwa wakulima,wafanyabiashara na makampuni madogo Nchini kujiandaa na kushiriki maonesho ya Kilimo na Sikukuu ya Wakulima NaneNane ya Kanda ya Ziwa Mashariki ili kujifunza teknolojia mpya kutoka katika makampuni ya nje.
Maonesho hayo ambayo mwaka 2018 yanatarajia kufanyika kitaifa Mkoani Simiyu yameelezwa kuwa yatakuwa ya kipekee ikilinganishwa na miaka mingine huku yakitoa fursa zaidi kwa wafanyabiashara na makampuni madogo kujitokeza kwa wingi kushiriki.
Akizungumza leo Aprili 12 katika kikao cha maandalizi ya Nane Nane Kitaifa yanayotarajiwa kufanyika Mkoani Simiyu, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Edwin Rutageruka amesema kuwa taasisi yake iko tayari kutoa ushirikiano wa dhati kwa uongozi wa Mkoa wa Simiyu ili kuhakikisha wanayafanya maonesho hayo kuwa ya kipekee.
Amesema ni vema makampuni madogo, wakulima na wafanyabiashara wakajitokeza kushiriki maonesho hayo kwani watapata fursa ya kujifunza Teknolojia mpya kutoka nchi za nje ambazo zitashiriki maonesho hayo.
“Ni vema Wafanyabiashara, wakulima na makampuni madogo yakajitokeza kushiriki maonesho hayo kwani tumejipanga vizuri, tumetenga maeneo mazuri na tutapanga kulingana na sekta mbalimbali ”alisema
Ameongeza kuwa katika kuyatangaza maonesho hayo ya Nane Nane ya mwaka huu 2018 , TanTrade itaandaa dawati maalum la kuutangaza rasmi Mkoa wa Simiyu na fursa zilizopo ili Watanzania na Wawekezaji wajitokeze kwa wingi kuwekeza.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amesema uwepo wa Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Ziwa Mashariki yatakayofanyika Mkoani humo, kwa kushirikiana na Mikoa ya Mara na Shinyanga ambayo kwa pamoja inaunda Kanda hiyo, yatasaidia wakulima kujifunza kwa washiriki kutoka maeneo mbalimbali na hatimaye kuongeza thamani ya mazao yao.
Mtaka ameeleza kuwa mbali na Uwanja wa Maonesho kutumika kwa ajili ya Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Nane Nane, Uwanja huo utatumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo zitawanufaisha kiuchumi wananchi na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Bahini Masunga amesema kuwepo kwa Maonesho ya Nane Nane kutawasaidia Wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kutambua fursa mbalimbali pamoja na kujiongezea ujuzi wa namna ya kuongeza thamani katika bidhaa zao.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA HAPA:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/04/mkurugenzi-tantrade-atoa-wito-kwa.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa