Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kupitia Mkoa wa Mara, Christopher Gachuma amewaongoza wananchi na viongozi wa CCM na Serikali wa mkoa wa Simiyu katika mazishi ya aliyewahi kuwa mbunge wa Bariadi Mashariki , Mkuu wa Wilaya katika maeneo mbalimbali hapa nchini,ambaye pia alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Simiyu, Bw. Danhi Makanga, ambayo yamefanyika katika Mtaa wa Kidulya Mjini Bariadi .
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Taifa, Gachuma ametoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wote walioguswa na msiba huo, huku akiwaasa ndugu na familia kuendelea kuishi maisha ya umoja na kushirikiana.
Aidha, Gachuma amepongeza mkoa wa Simiyu kwa ushirikiano uliopo kati ya Viongozi wa Chama na Serikali katika masuala yote ikiwa ni pamoja na misiba na akikiri kuwa yeye pamoja na baadhi ya viongozi wa mkoa wake(Mara) walioongozana naye wamejifunza jambo hilo kutoka Simiyu.
"Napenda niupongeze uongozi wa mkoa wa Simiyu kwa namna mnavyoshirikiana, msiba wa ndugu yetu Makanga mmeubeba wote kwa pamoja tumeona kuna umoja na ushirikiano kati ya viongozi wa Chama na Serikali hili ni jambo jema sana , bahati nzuri nimefuatana na Katibu Mwenezi wangu wa Mkoa utaratibu huu na sisi tunaubeba kama somo" alisema Gachuma.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo akitoa salamu za rambirambi ametoa pole kwa familia na kuwaomba ndugu na familia waendelee kuwa wamoja na wasikubali kugawanywa kwa namna yoyote, huku akielezea kuwa CCM imempoteza mtu muhimu makini sana ambaye alikuwa na mchango mkubwa katika Chama, Serikali na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Yakobo amewashukuru viongozi wa CCM Taifa kwa kutuma mwakilishi, pia akawashukuru wananchi, viongozi wa Chama na Serikali mkoani Simiyu kwa namna walivyoonesha umoja na ushirikiano katika msiba wa Bw. Danni Makanga hali ambayo imeleta heshima kwa Chama na kumfanya marehemu Makanga kuzikwa kwa heshima kama kiongozi wa Chama.
Akimzungumzia marehemu Danni Makanga, Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kadogosa amesema tangu marehemu akiwa Mbunge wa Bariadi na Mkuu wa Wilaya katika maeneo mbalimbali na kubainisha kuwa alikuwa kiongozi ambaye kupitia yeye vijana wa sasa wanaweza kujifunza namna ya kuitumikia Serikali na wananchi kupitia yeye.
Naye Mkuu wa Wilaya mstaafu, Malietha Sanka ambaye alifanya kazi na marehemu wakati wa uhai wake amesema atamkumbuka Marehemu Danni Makanga kwa uchapakazi wake, huku akimwelezea kuwa wakati akiwa mbunge aliwahi kuwa mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo alisaidia kutatua mambo mbalimbali kupitia chombo hicho cha maamuzi katika chuo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa pole kwa familia, ndugu na marafiki wa marehemu Danni Makanga huku akisisitiza kuwa viongozi wa Chama na Serikali Mkoani humo wameonesha ushirikiano tangu walipopata taarifa za msiba mpaka wakati wa mazishi ili kumsindikiza marehemu aliyekuwa kiongozi katika heshima zote za Chama na Serikali.
Akitoa mahubiri wakati wa ibada ya mazishi, Padri wa Kigango cha Mtakatifu Michael Kidulya, Parokia ya Mtakatifu Luka Bariadi, James. Kitasanja amewaasa watu wote kujiandaa kwa kuwa hakuna ajuaye siku ya kufa kwake, huku akiwasisitiza kushika maagizo ya Mungu ikiwa ni pamoja na kuwapenda na kuishi vizuri na watu wote.
Marehemu Danni Makanga alifariki Juni 23 katika ajali iliyohusisha lori na pikipiki Mkoani Mwanza, ambapo wakati wa uhai wake aliwahi kuwa mbunge, mkuu wa wilaya na mpaka mauti inamkuta alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Simiyu, ameacha mke na watoto watano.
MWISHO
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa