Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde amezindua rasmi Maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria ambayo yanafanyika Kitaifa
Mkoani Simiyu na kutoa wito kwa viongozi wa Serikali kuwatumia wasajili wasaidizi na watoa huduma za kisheria kutatua matatizo ya kisheria yanayowakabili wananchi.
Akizungumza na wananchi Oktoba 21, 2019 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simyu Mavunde amesema matatizo ya kisheria yanashughulikiwa kisheria na siyo kisiasa hivyo ni vema wakawashirikisha na wakaambatana nao hata katika ziara zao ili waweze kutoa msaada wa kisheria kila unapohitajika.
“Yapo mambo mengi sana ambayo ni ya kisheria wananchi mmekuwa mkikimbilia kwa viongozi wa kisiasa, siasa ina sehemu yake inakoma inabaki sheria, wiki ya msaada wa kisheria ni fursa ya kipekee kuelewa namna ya kushughulikia matatizo yenu na mnaendelea kujifunza kuwa sheria inabaki kuwa sheria na utatuzi wake unakuwa katika mfumo uliowekwa kisheria,” alisema Mavunde.
Awali akitoa taarifa ya wiki ya msaada wa kisheria Msajii wa Taasisi za watoa huduma za kisheria, B. Felistas Mushi amesema lengo la kuwepo wa huduma ya msaada wa kisheria ni kuhakikisha haki inapatikana kwa wananchi wasioweza kumudu gharama za wawakili”tunaamini kuwa baada ya maadhimisho haya kutakuwa na mtazamo chanya katika kutatua matatizo ya wananchi kisheria.”
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe Anthony Mtaka ametoa wito kwa viongozi wa Mkoa wa Simiyu wahakikishe katika ziara zao wanaambatana na wasajili wasaidizi na watoa huduma za kisheria walio katika maeneo yao ili waweze kutatua na kutoa ushauri wa namna ya kutatua matatizo yote kisheria.
Aidha, amewataka viongozi na wajumbe wa mabaraza ya ardhi ya vijiji, kata na wilaya kuhakikisha kuwa wanatumia vizuri mafunzo wanayopewa na wakayatafsiri kwa vitendo katika utatuzi wa matatizo ya watu kwa haki na kushirikiana na viongozi wa Serikali, taasisi na vyombo vyote vya maamuzi.
Katika hatua nyingine Mtaka ameshauri kuwa ingekuwa vema pia kama masuala ya kisheria yakajumuishwa katika baadhi ya masomo kama vile somo la Uraia ili kuendelea kujenga uelewa wa pamoja juu ya namna ya kukabiliana na matatizo yote ya kisheria.
Kwa upande wake Mkuugenzi Mtendaji wa TANLAP, Bi. Christina Ruhinda ameiomba Serikali na taasisi zake kushirikiana na watoa huduma za kisheria ili huduma hizo ziwe endelevu na matatizo ya wananchi yaweze kufanyiwa kazi kwa haki.
Mkurugenzi wa Miradi Shirika la Legal Services Facility, Bi. Scholastica Jullu amesema shirika ilo litaendelea kufadhili mashirika yanayotoa msaada wa kisheria kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa kisheria mwaka 2019 yanaongozwa na Kauli Mbiu “Msaada wa Kisheria kwa Maendeleo Endelevu”, wakati yakiadhimishwa kitaifa mkoani SIMIYU yanapotarajiwa kuhitimishwa Oktoba 25, 2019 pia yanaadhimishwa katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Iringa, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro,Mbeya, Mtwara, Mwanza, Njombe, Ruvuma, Shinyanga, Tabora na Tanga.
MWISHO
KUPATA PICHA ZADI FUNGUAA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/10/naibu-waziri-mavunde-awataka-viongozi.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa