Wilaya ya Maswa imezindua mfuko wa walimu kwa lengo la kuwasaidia walimu ambao hawana sifa za kukopesheka katika taasisi zingine za fedha ili waweze kupata mikopo kwa riba nafuu.
Mfuko huo umezinduliwa na Katibu wa Chama cha Walimu nchini, Mwl. Deus Seif wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu zaidi ya 1400 wa shule za msingi 123 za wilaya hiyo kwa kuwezesha wilaya kufanya vizuri kwenye Matokeo ya darasa la saba na kuongeza ufaulu kutoka asilimia 34.9 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 88.73 mwaka 2019.
Akizungumza na mamia ya walimu walioshiriki katika uzinduzi huo, Seif amewaasa walimu kutambua thamani waliyopewa na viongozi wa wilaya na mkoa kwa kuendelea kuwajibika kwa uadilifu mkubwa.
“ Nitoe wito kwa walimu wenzangu ambao si waadilifu wabadilike, wale watoro waache utoro, ambao ni walevi wache ulevi wafundishe watoto; lakini wazazi na ninyi mtusaidie kuhimiza watoto wawe na mahudhurio mazuri shuleni ili walimu waweze kufanya kazi yao vizuri,” alisema Seif.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Dkt. Fredrick Sagamiko amesema hadi sasa mfuko huo umeingiziwa kiasi cha shilingi milioni 15 na halmashauri na baadaye wadau kuongeza kiasi cha shilingi milioni 15 na kuufanya mfuko huo kuwa na jumla ya shilingi milioni 30.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Antony Mtaka amewataka walimu kuacha tabia ya kukopa fedha katika taasisi nyingine za fedha hususani za binafsi zenye riba kubwa ambazo huwalazimu kuweka kadi zao za benki kama rehani, huku akishauri Benki ya walimu kuja na huduma zinazojibu changamoto za walimu ikiwemo kutoa mikopo kwa riba nafuu
Kwa upande wake Katibu wa CWT ameipongeza Wilaya ya Maswa kwa kuona haja kuwapongeza walimu na ya kuwasaidia walimu kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu kupitia mfuko huo, ambapo CWT pia imeunga mkono juhudi Wilaya kwa kuchangia kiasi cha shilingi milioni Nane (8).
Wilaya hiyo pia imetoa zawadi ya majiko ya gesi 101 kama zawadi kwa shule hizo ili kuwawezesha walimu kupata chai asubuhi wakiwa shuleni na kuwapunguza walimu muda wa kwenda kutafuta huduma hiyo nje ya maeneo ya shule.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Seif Shekalaghe amesema mwaka 2018 Wilaya ilitoa majiko ya gesi kwa shule 20 zilizofanya vizuri hivyo, majiko hayo yanatolewa kwa shule 101 ambazo hazikupata awali, pamoja na zawadi ya majiko shule zilizofanya vizuri zimepewa fedha taslimu shilingi 500,000.
Katika uzinduzi huo pia ilifanyika harambee kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa nyumba nne za walimu ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa nyumba za walimu
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/11/maswa-yazindua-mfuko-wa-walimu.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa