Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Adam Malima amesema Mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga inayounda Kanda ya Nanenane ya Ziwa Mashariki imekusudia kuboresha zaidi maonesho ya Nanenane Kitaifa mwaka 2019 ambayo yanafanyika kwa mara ya pili sasa katika kanda hii kwenye Viwanja vya Nyakabindi Bariadi Mkoani Simiyu.
Malima ameyasema hayo jana katika kikao maalum cha maandalizi cha Kanda hiyo kilichofanyika kwa lengo la kutathmini hali ya maandalizi ya maonesho hayo ambayo yanatarajia kuanza tarehe 29 Julai, 2019 na kuhitimishwa rasmi Agosti 08, 2019.
Amesema kanda imekusudia kuboresha upatikanaji wa huduma za maji, umeme na miundombinu mingine muhimu ikiwa ni pamoja na kuongeza majengo ya kudumu ili katika siku za usoni kanda ya Ziwa Mashariki iwe sehemu ya kudumu ya maonesho ya Kilimo Biashara.
“Mwaka huu tumekusudia kuboresha maonesho ya Nanenane Kitaifa kuliko mwaka jana 2018, tumekubaliana kuboresha upatikanaji wa huduma katika maeneo ya viwanja vua maonesho na pia tunakusudia kuongeza upatikanaji wa majengo ya kudumu kwa sababu kwa kadri tunavyokwenda tunatarajia hapa iwe ni sehemu ya Maonesho ya Kilimo Biashara kwa kanda hii” alisema
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema Maonesho ya Nanenane mwaka 2019 yatakuwa na waoneshaji wengi wa teknolojia za kilimo kuliko miaka iliyopia, hivyo akawahakikishia wananchi wote kuona teknolojia mbalimbali ikiwa ni pamoja na za upukuchuaji, utengenezaji wa chakula cha mifugo, ukataji majani ya mifugo, uvunaji na teknolojia nyingine nyingi.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao Wizara ya Kilimo, Bw. Nyasebwa Chinagu amesema moja ya jukumu la wizara hiyo katika Maonesho haya ni kuhakikisha kuwa teknolojia sahihi zilizopo zinaoneshwa katika Maonesho ya nanenane ili wakulima, wafugaji na wavuvi waweze kupata maarifa na teknolojia sahihi katika kuongeza tija katika uzalishaji.
Maonesho ya haya yanatarajiwa kufunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wa Kitaifa watakuwepo katika siku maalum, akiwepo Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda na mgeni rasmi katika kilele cha maonesho haya anatarajiwa kuwa Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanafanyika kwa mara ya pili sasa mkoani Simiyu chini ya kauli Mbiu:-“KILIMO, MIFUGO NA UVUVI KATIKA UKUAJI WA UCHUMI WA NCHI” tangu Kanda ya Ziwa ilipogawanywa katika kanda mbili yaani, Kanda ya Ziwa Mashariki(Simiyu, Mara na Shinyanga) na Kanda ya Ziwa Magharibi(Mwanza, Geita na Kagera).
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGNISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/07/maonesho-ya-nanenane-kitaifa-2019.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa