Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi. Stella Manyanya ametoa wito kwa wananchi kushiriki katika Maonesho ya Nanenane kwa lengo la kujifunza ili waongeze tija katika uzalishaji, huku akibainisha kuwa maonesho haya yameboreshwa, kwa wadau na Taasisi zinazotoa huduma kuongezeka na maonesho hayo kuwa sura ya kuwasaidia wananchi kubadilika.
Mhandisi Manyanya ameyasema hayo Agosti 02, 2019 kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa mwaka 2019 yanayofanyika Kanda ya Ziwa Mashariki viwanja vya Nyakabindi Bariadi mkoani Simiyu.
“ Maonesho ya mwaka huu yamefana sana na kufana kwake hakupo katika namna mahema yalivyo, bali ushiriki wa waoneshaji, wakulima wenyewe na nimefurahi kuona baadhi ya mambo yanafanyika kwa vitendo kama uhimilishaji wa ng’ombe, ufugaji wa samaki, uwepo wa taasisi kama TBS, Wakala wa vipimo na vyama vya ushirika”
“ Mimi naona tumeboresha zaidi namna ya kufanya haya maonesho kwenda zaidi katika sura ya kuwagusa wananchi ili waweze kubadilika na kutumia huduma zinazohitajika, nipende kuwashawishi wananchi wengi zaidi wasikose kuja kujifunza kupitia maonesho haya, wanapojifunza wanaongeza tija katika maeneo yao” alisisitiza Mhandisi. Manyanya.
Aidha, amezihamasisha Halmashauri zote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na uwekezaji mwingine ili wawekezaji wanapopatikana kusiwe na mlolongo mrefu katika kupata ardhi na kupata vibali mbalimbali, huku akibainisha kuwa Serikali imeshaweka miundombinu wezeshi kwa uwekezaji kama upatikanaji wa umeme.
Amesema sekta binafsi ndiyo injini ya ukuaji wa uchumi katika Taifa hasa kwenye eneo la biashara na viwanda huku akiongeza kuwa ni vyema maonesho hayo yakawa na kiu ya kufanya mambo yatakayoweza kurahihisha shughuli za kibiashara.
Awali Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema wananchi wengi wa Mkoa wa Simiyu wanajishughulisha na shughuli za kilimo hivyo ipo haja ya kuwepo kituo endelevu cha mafunzo ya kilimo ili wakulima waweze kupata mahala pa kujifunzia .
“Kutokana na kwamba wananchi wengi wa Mkoa wa Simiyu wanategemea sana hasa shughuli za kilimo ipo haja ya kuwepo kituo endelevu kwa ajili ya mafunzo kitachowasaidia wakulima kupata elimu kila siku kutokana na uhitaji wao”.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa wananchi na wajasiriamali wa mkoa wa Simiyu kutembelea Viwanja vya Nanenane kwa lengo la kujifunza kutoka kwa wenzao kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu namna wanavyofanya shughuli zao na namna walivyofanikiwa.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/08/manyanya-atoa-wito-kwa-wananchi.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa