Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi. Stella Manyanya amesema ameridhishwa na Maandalizi ya Maonesho ya Viwanda Vidogo (SIDO) Kitaifa, yatakayofanyika kuanzia Oktoba 23-28, 2018 katika Viwanja vya Nyakabindi Bariadi Mkoani Simiyu na kutoa wito kwa wananchi kushiriki maonesho hayo, ili kujionea teknolojia na mashine rahisi zitumikazo kuongeza thamani bidhaa mbalimbali.
Mhandisi Manyanya amesema pamoja na kuwepo wa teknolojia na mashine, wajasiriamali kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini wameshawasili kwa ajili ya kuja kuonesha bidhaa mbalimbali wanazozalisha hivyo.
“Nitumie nafasi hii kuwapongeza viongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa maandalizi mazuri nimeridhishwa na maandaizi na niwaombe wananchi waMkoa wa Simiyu na maeneo mengine kufika katika maonesho ya kwanza ya Kitaifa ya Viwanda Vidogo, kupata teknolojia na mashine rahisi tunazozitumia katika kuongeza thamani za bidhaa zetu hapa nchini” alisema
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo SIDO, Prof. Sylvester Mpanduji amesema wajasiriamali zaidi ya 1000 kutoka mikoa yote hapa nchini wnatarajia kushiriki maonesho haya,
Aidha, Profesa Mpanduji amesema ametoa wito kwa wananchi kwenda kuona teknolojia mbalimbali rahisi ambazo watazitumia kuanzisha viwanda, huku akibainisha kuwa shirika hilo litahakikisha viwanda vyote vinavyoanzishwa na Watanzania vinakuwa ili ifikapo mwaka 2025 nchi iwe na viwanda vikubwa vinavyoendeshwa na Watanzania.
Nao Wajasiriamali kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini wameeleza matumani yao kupitia Maonesho haya katika kuona teknolojia mpya katika utengenezaji wa bidhaa zao, kujifunza kutoka kwa wenzao na kuboresha bidhaa zao pamoja na kuongeza wigo wa masoko ya bidhaa zao.
“Haya ni maonesho ya kwanza kufanyika Kitaifa nina imani yatakuwa makubwa kuliko tulikuwa tukifanya awali, nina matumaini makubwa kuwa nitakutana na wajasiriamali wenzangu na kujifunza mengi kwao, kukutana na wananchi wa Simiyu na maeneo mengine nikauza bidhaa zangu zote zikaisha” alisema Hapyness Mabula kutoka mkoa wa Mwanza.
“ Katika maonesho haya natarajia kujifunza mambo mengi sana kwa sababu ni ya Kitaifa tofauti na yale tuliyokuwa tunaonana kikanda,naamini nitatanua wigo wa wajasiriamali nitakaokutana nao pamoja na soko la bidhaa zangu ninazozalisha” alisema Hamisi Samade kutoka mkoa wa Singida.
Katka hatua nyingine wajasiriamali hao wameomba Serikali iwasiadie katika upatikanaji wamitaji na kutatua changamoto zinazowakabili mipakani wanaposafirisha bidhaa zao wanazozalisha au malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa bidhaa zao..
Maonesho ya SIDO Kitaifa yatafunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa na yanatarajiwa kuhitimishwa na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein.
MWISHO
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa