Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amewataka Maafisa Michezo na Walimu wa Michezo mkoani humo kuwasaidia Vijana wa Kitanzania kutoka kwenye nadharia ya kufikiri kuwa michezo ni afya, urafiki na burudani tu ili waanze kufikiri michezo katika mtazamo wa biashara na ajira.
Mtaka ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunga semina ya kuwajengea uwezo Maafisa Michezo, Viongozi wa Vyama na Vilabu vya Michezo, makocha na walimu wa michezo shuleni, kwa lengo la kuchochea maendeleo ya Michezo Mkoani Simiyu, ambayo yametolewa na Dkt. Angela Daalmann na Anja Henke ambao ni Wataalam wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover Nchini Ujerumani.
“Tumeleta mafunzo haya tukiamini kuwa Maafisa Michezo wote ndani ya Mkoa wa Simiyu watakuwa na msaada mkubwa kwenye kuwaandaa vijana wa Kitanzania kutoka kwenye nadharia ya kusema michezo ni afya, michezo ni upendo, michezo ni burudani ; nataka Afisa Michezo akienda kwenye implementation(utekelezaji) vijana wa mkoa wa Simiyu waanze kujenga vichwani mwao kuwa michezo ni ajira, michezo ni biashara” alisema Mtaka.
“Katika Dunia ya leo michezo ni biashara kubwa na ni ajira kubwa ya dunia ndiyo maana hapa mmefundishwa kuhusu miradi, hili suala la michezo ni burudani, michezo ni afya, michezo ni urafiki na upendo libaki kama jambo la pili” alisisitiza
Ameongeza kuwa Maafisa Michezo pamoja na walimu wa michezo Mkoani Simiyu kupitia michezo ya UMITASHUMTA na UMISETA wanapaswa kuwatambua watoto/vijana wenye vipaji na kuwaandaa kibiashara ili wajue kuwa vipaji vyao ni ajira zao za baadaye.
Aidha, amesema Serikali mkoani humo imedhamiria kutangaza utalii na kukuza uchumi kupitia sanaa, michezo na utamaduni na akabainisha kuwa Mkoa umeanza kutekeleza hilo kupitia uanzishwaji wa Tamasha kubwa la michezo na utamaduni maarufu kama “Simiyu Festival” ambalo linafanyika kila mwaka na kwa mwaka 2018 litafanyika mapema mwezi Julai.
Naye Mtalaam wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover Dkt. Angela Daalmann amesema kwamba wamehamasika kutoa mafunzo kwa maafisa, viongozi na walimu wa michezo mkoani Simiyu ikiwa ni mara ya pili sasa, kutokana na utayari wa viongozi na watalaam mkoani humo katika kuleta mapinduzi kwenye sekta ya michezo.
Afisa Michezo wa Mkoa wa Simiyu, Bw.Emmanuel Athanas amesema mafunzo hayo yataamsha ari na hamasa ya michezo kwa Maafisa Michezo na Walimu wa Michezo mkoani humo na kuwasaidia katika kuibua miradi mbalimbali itakayohusianishwa na michezo (sports projects) sambamba na kuwatafuta wadau mbalimbali kuwezesha miradi hiyo.
Naye Afisa Michezo wilaya ya Meatu, Bw. Hassan Sengulo amesema mafunzo hayo yamewasaidia kutambua namna sahihi ya kupata fedha kwa ajili ya uendeshaji wa michezo, hivyo watayatumia kuwaelimisha Walimu wa Michezo na Viongozi wa Vyama na Vilabu vya Michezo namna ya kutatua changamoto ya ukosefu wa fedha za kuendeshea michezo.
Semina hii ilijumuisha jumla ya washiriki 27 kutoka Halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu na baadaye ikafuatiwa na Bonanza la michezo kwa wanafunzi wa baadhi ya shule za msingi kushiriki mchezo wa riadha, ambapo wanafunzi walipata nafasi ya kukimbia mbio za mita 100, mita 400 na mita 1500 katika Uwanja wa Shule ya Msingi Somanda Mjini Bariadi.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA HAPA:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/03/maafisa-michezo-watakiwa-kuwasaidia.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa