Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Khamis Kulemba ameutaka uongozi wa Kituo cha Afya Lukungu wilayani Busega kuimarisha ukusanyaji na usimamizi wa mapato (kudhibiti upotevu wa mapato) ili kuongeza mapato yatakayosaidia kununua dawa na kuboresha miundombinu kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Dkt. Kulemba ameyasema hayo Septemba 10, 2020 katika nyakati tofauti wakati wa ziara ya usimamizi shirikishi iliyofanyika katika kituo hicho, ambapo moja ya malengo ya ziara ilikuwa ni kukagua mifumo ya ukusanyaji wa mapato na hali ya utoaji wa huduma za afya kwa ujumla wake.
“Imarisheni mfumo wa ukusanayaji mapato nataka wakati ujao mapato yaongezeke mara mbili ya sasa, mkumbuke kuwa kwa kadri tunavyodhibiti upotevu wa mapato ndiyo tutakavyoboresha utoaji wa huduma; tutaweza kununua dawa na kufanya maendeleo ya kituo chetu hali itakayochangia kuongeza ufanisi katika huduma zinazotolewa kwa wananchi,” alisema Kulemba.
Ameongeza kuwa Uongozi wa Kituo hicho unapaswa kuhakikisha kuwa mfumo wa GoT-HOMIS unaohusika na usimamizi na uendeshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya unafungwa na kufanya kazi kituoni hapo, ili kudhibiti aina yoyote ya upotevu wa mapato kwa kuwa taarifa ya kila huduma na mapato zitaingizwa katika mfumo huo.
Naye Afisa Afya kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu amesema pamoja na kuimarisha mfumo wa mapato uongozi huo uboreshe mazingira kwa kusafisha mara kwa mara maeneo ya kituo hicho pamoja na kupanda bustani za maua.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa idara ya afya wilaya ya Busega, Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya amesema watatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na mganga mkuu wa mkoa ili kutimiza azma ya serikali ya kutoa huduma zinazotakiwa kwa wananchi na kwa wakati.
Baadhi ya wananchi waliopata huduma za matibabu katika kituo cha afya Lukungu wameupongeza uongozi wa kituo kwa namna ulivyoboresha utoaji wa huduma na kuomba hali ya upatikanaji wa dawa iimarishwe zaidi na miundombinu ya kutoa huduma ikiwemo huduma za upasuaji, wodi za kulaza wagonjwa ziongezwe ili wapate huduma zote kituoni hapo.
“ Kwa upande wa huduma mimi nimehudumiwa vizuri, nimepokelewa vizuri na wauguzi wamenisikiliza baada ya kunisikiliza nimeenda kwenye vipimo na nilivyorudi kwa daktari amenieleza tatizo langu akaniandikia dawa, nashukuru dawa zote nilizoandikiwa nimepewa,” Mandege William Manyama, mkazi wa Kijiji cha Lukungu.
“Huduma zote nilizokuwa nazihitahitaji nimezipata na nimehudumiwa ndani ya muda mfupi, ombi langu serikali ione namna ya kuongeza huduma hasa za kulaza wagonjwa ili tuipate hapa hapa badala ya kupelekwa kwenye vituo vingine na hospitali,” alisema Daud Moshi mkazi wa Kijiji cha Lukungu.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2020/09/kituo-cha-afya-lukungu-chatakiwa.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa