Katibu Tawala wa Mkoawa Simiyu, Bibi. Miriam Mmbaga ametoa wito kwa viongozi, walimu, wazazi na wadau wote wa elimu mkoani hapa kushiriki kikamilifu katika kutekeleza na kuwezesha azma ya mkoa ya kuwa nafasi ya kwanza katika mitihani yote ya Taifa.
Mmbaga ameyasema hayo Desemba 09, 2020 Mjini Bariadi wakati akifungua kikao cha viongozi, watendaji na wadau wa elimu mkoa cha kutangaza Mkakati wa Mkoa wa kuboresha taaluma kwa mwaka 2021 ambapo alibainisha kuwa endapo kila mdau atatimiza wajibu wake Simiyu itakuwa mkoa bora katika elimu.
“Mkoa wetu kushika nafasi ya kwanza inawezekana kabisa, kama tuliweza kutoka nafasi za mwishoni kabisha tukaingia, kumi bora, sasa hivi tuka katika tatu bora, naamini kwa uweza wa Mwenyezi Mungu tunaweza kushika nafasi ya kwanza katika mitihani yote ya Taifa,” alisema Mmbaga.
Aidha, Mmbaga amewataka viongozi wa idara ya elimu kuepuka kutumia kauli chafu kwa walimu kwa kuwa zinawakatisha tamaa na kupunguza tija na ari katika utendaji kazi wao badal yake watumie mbinu sahihi za kiuongozi kutatua changamoto wanazoziona kwa walimu.
Naye Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest Hinju amesema ushirikiano, mawasiliano na mahusiano mazuri baina ya walimu, viongozi na wadau wote wa elimu yanasaidia muda mwingi kutumika kufundisha na kusimamiana badala ya kutumika kuzozana, kugoma na kusuluhishana.
Baadhi ya walimu na Maafisa Elimu wa Kata na Halmashauti wamesema wameupokea mkakati huo na kuahidi kutimiza wajjibu wao ili kuweza kufikia malengo ya mkoa na kuboresha taaluma na elimu mkoani Simiyu huku wakitoa maoni mbalimbali namna ya kuboresha zaidi utekeelzaji wa mkakati huo.
“Nashauri mkoa uanzishe mitihani ya pamoja ya madarasa tarajiwa yaani darasa la tatu, darasa la sita, kidato cha kwanza na kidato cha tatu, mitihani hii itusaidia kujua shule zipi zina changamoto gani na itasaidia kuweka mikakati ya kuziwezesha kufanya vizuri kwa kuwa walimu na viongozi wengine watakuwa na mwaka mzima wa kuyaandaa madarasa hayo kabla ya mtihani wa Taifa,” alisema Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Lagangabilili Itilima, Mwede Hongoa.
“Tunaomba Serikali iboreshe makazi ya walimu, walimu wengi hawana nyumba za kuishi maeneo ya shule wengi wanatoka mbali na Shule hivyo wakati tunapohitaji kuwasaidia wanafunzi hasa nyakati za usiku inakuwa vigumu kwao kushiriki kikamilifu,” alisema Mwalimu Flora Shimbi Mkuu wa Shule Itilima Sekondari.
“Serikali ya Mkoa imetoa motisha kwa walimu hasa wanaofanya vizuri na walimu wa mkoa wa Simiyu wamehamasika sana na wanajituma katika kazi yao, tunaomba serikali iendelee kuboresha miundombinu ikiwemo vyumba vya madarasa, madawati na viti ili mazingira yao ya kufundishia yawe bora zaidi,” alisema Mwalimu Oscar Nsolo Mkuu wa Shule Sapiwi Sekondari.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo ameshauri mkoa wa Simiyu kuwa na mfuko wa elimu wa mkoa, ili mfuko huo uweze kusaidia katika ujenzi wa miundombinu ya elimu huku akitoa wito kwa wazazi na wadau wote wa elimu kuona umuhimu wa kuuchangia mfuko huo.
Mkakati wa kuboresha taaluma mkoa wa Simiyu kwa mwaka 2021 umejumuisha mambo muhimu ikiwa ni pamoja na Uwezo wa kujituma kwa viongozi wa elimu, uungwaji mkono na viongozi wa juu,uwajibikaji wa maafisa elimukata na mfumo wa utawala, huduma bora na mawasiliano kwa walimu/wadau wa elimu, utoaji wa motisha na zawadi, ufatiliaji kabambe wa ufundishaji na ujifunzaji, mafunzo kazini,upimaji, miundombinu na samani, kambi za kitaaluma, matumizi ya mitandao ya TEHAMA.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2020/12/kila-mdau-awe-sehemu-kuufikisha-mkoa.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa