Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka wa Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Richard Mayongela ameiomba serikali kutoa kiupaumbele cha ujenzi wa Viwanja vya Ndege kwa mikoa ya Simiyu na Lindi katika bajeti ya mwaka 2018/2019 ili kuongeza fursa za uwekezaji na utalii.
Mayongele ametoa ombi hilo leo katika kijiji cha IGEGU kata ya Sapiwi wilayani BARIADI katika eneo linalotarajiwa kujengwa Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Simiyu, wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa mkoani Simiyu.
Amesema hatua za awali za maandalizi ya ujenzi wa Uwanja huo zimekamilika ambapo usanifu na upembuzi yakinifu vimeshafanyika na makadirio ya awali yanaonesha kuwa mradi huo utagharimu takribani shilingi bilioni 95.56 na utakapokamilika utawezesha ndege zenye uwezo wa kubeba kuanzia watu 75 na kuendelea kutua.
Ameongeza kuwa Ujenzi wa Uwanja huo utakapokamilika utakuwa ni chachu ya maendeleo kwa Mkoa huo katika nyanja za uchumi na utalii na utachangia kuufungua mkoa wa Simiyu kiuchumi pamoja na mikoa mingine ya kanda ya Ziwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema kukamilika kwa Uwanja huo itakuwa ni faida kubwa kwa kuwa utakuwa Uwanja pekee wa Serikali hapa nchini ambao Watalii watautumia kuifikia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa urahisi kuliko viwanja vingine.
“Tunajenga Uwanja ambao kimkakati unakaa mpakani mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, karibu na uwanja huu kuna hii barabara ya inayotunganisha na Mkoa wa Shinyanga kupitia Malampaka ambako kutajengwa Reli ya Kisasa, hapa jirani tuna eneo ambalo tutajenga Kiwanda cha Vifaa tiba, mbele yeke tunaanzisha Kanda ya Nanenane ...tunaamini kukamilika kwa mradi huu kutakuwa na faida sana kwa Serikali na wananchi” alisema Mtaka
Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewahikikishia viongozi wa Mkoa wa Simiyu juu ya ujenzi wa uwanja wa ndege Simiyu, lakini akatoa angalizo kuwa wakati kufanya tathmini ya fidia ya eneo la ujenzi, gharama ya fidia isiwe kubwa vinginevyo Uwanja huo hautaweza kujengwa.
“Wale watakaokuja kufanya tathmini wahakikishe gharama ya fidia inakuwa chini sana na ifanywe kwa mujibu wa sheria, hatutaweza kuwadhulumu watu lakini tuhakikishe tathmini inafanyika kwa mujibu wa sheria” alisisitiza Waziri Mbarawa.
Akizungumza kwa niaba ya Wananchi wa Kijiji cha Igegu mahali unapotarajiwa kujengwa uwanja huo, Diwani wa Kata ya Sapiwi, Mhe.Kibuga Gamalieli amesema wananchi wanasubiria kwa shauku kubwa kuona Uwanja huo unakamilika na akamuhakikishia Waziri Mbarawa kuwa wananchi hawatadai fidia kubwa katika eneo hilo kwa kuwa wanataka maendeleo.
Waziri Mbarawa yuko Mkoani Simiyu kwa ziara ya siku mbili ambapo leo pamoja na kutembelea eneo la ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mkoa Simiyu amezungumza na watumishi wa Taasisi zote zilizo chini ya Wizara yake, amekagua Ujenzi wa Hospitali ya Mkoa na Nyumba za Viongozi wa Mkoa na kutembelea Kambi ya Mkandarasi wa Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Bariadi-Maswa kata ya Luguru wilayani Itilima
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA HAPA:https://simiyuregion.blogspot.com/2018/02/kaimu-mkurugenzi-wa-viwanja-vya-ndege.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa