Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa(SUMA JKT), Luteni Kanali Peter Lushika amesema JKT limedhamiria kuwafundisha wananchi watakaofika Uwanja wa Nanenane Nyakabindi Bariadi Mkoani Simiyu, teknolojia mbalimbali za ufugaji wa samaki ikiwa ni pamoja na ufugaji kwa kutumia mabwawa, matenki na vizimba(ndani ya ziwa), ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa samaki na kuzuia uvuvi haramu.
Luteni Kanali Lushika ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya hali ya maandalizi ya Jeshi hilo katika maonesho ya Nanenane Kitaifa mwaka 2018 na namna walivyojipanga kutoa elimu wa wananchi katika maeneo mbalimbali hususani katika kilimo, ufugaji na uvuvi.
“Tunajua wengi wanafahamu ufugaji wa samaki kwenye mabwawa, mwaka huu tunawaletea teknolojia ya ufugaji wa samaki kwenye matenki, walioko ziwani tutaonesha ufugaji wa samaki kwenye vizimba, teknojia hizi zitamsaidia mvuvi kuvua kuwa na uhakika wa upatiakanaji wasamaki, uhifadhi wa mazingira na kuondokana na uvuvi haramu” alisema Luteni Kanali Lushika.
Amesema JKT itawaeleza wananchi kuwa ufugaji wa samaki ni njia pekee ya kumwezesha mvuvi kupata samaki wakati wowote atakaohitaji hasa ufugaji kwa kutumia matenki.
Ameongeza kuwa pamoja na kuona teknolojia hizo JKT itaandaa madarasa katika uwanja wa nanenane kwa ajili ya kufundisha wakulima, wafugaji, wavuvi, wajasiriamali ili waweze kuona mbinu za kilimo, ufugaji na uvuvi bora na matumizi bora ya pembejeo.
Katika hatua nyingine Luteni Kanali Lushika amesema ili kufikia Tanzania ya Viwanda lina mpango wa kuanzisha kiwanda cha kuchakata pamba ambacho kitachakata pamba kutoka ikiwa ghafi mpaka kufikia kwenye zao la mwisho ambalo ni nguo, hivyo kitaliongezea zaidi thamani zao la pamba.
Naye Luteni Joseph Lyakurya Meneja wa Mradi Sumaponics amesema teknojia ya kufuga samaki kwa kutumia matenki ni nzuri kwa kuwa inatumia eneo dogo la ardhi , maji kidogo lakini inakuwa na uwezo wa kuchukua samaki wengi ikilinganishwa na teknolojia ya mabwawa, hivyo akatoa wito watu wafike Uwanja wa Nanenane wajifunze.
Kwa upande wao Vijana wa JKT wamesema mafunzo waliyoyapata katika teknolojia mbalimbali yamewawezesha kupata maarifa ambayo yanaweza kuwasaidia kujiajiri wenyewe, hivyo wakatoa wito kwa wananchi kwenda kuona teknolojia hizo.
“Kama mtaalam wa masuala ya uvuvi niliyehitimu chuo cha uvuvi Kigoma, nikiwa JKT nimepata elimu ya vitendo zaidi ya kile nilichokipata chuoni, tukiwa hapa Nanenane Bariadi tutatoa elimu kuhusiana na masuala ya uvuvi kwa kutumia vizimba, nawaomba wananchi waje wajifunze, maana ufugaji wa samaki nao una tija katika Tanzania ya Viwanda” alisema Almasi Idd Yusuph kikosi cha 822 Lwamkoma JKT.
“Miimi nikiwa JKT nimejifunza namna ya kuandaa bustani kutokana na mafunzo niliyopata naweza kutambua udongo mzuri na ambao si rafiki kwa kilimo cha bustani kama huu, kupitia maonesho haya wananchi wataelewa ni namna gani wanaweza wakaufanya udongo huu ukafaa na wakalima bustani” alisema Nasri Mataka Kijana wa JKT 822 KK Lwamkoma Mara.
Naye Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa SUMA JKT Meja Peter Sebyiga amesema JKT inatoa huduma na kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa kuzingatia ubora , muda unaokubalika na jamii kwa bei rafiki kwa wateja, hivyo akatoa wito kwa wananchi kufika kwenye maonesho ya Nanenane ili kuona bidhaa hizo kutoka kwenye viwanda, kilimo, mifugo na uvuvi.
Meja Sebyiga ametoa wito kwa Taasisi, Makampuni na watu binafsi kutumia samani zinazotengenezwa na Kiwanda cha Jeshi la Kujenga Taifa kwa ajili ya matumizi ya Ofisi na nyumbani na kusisitiza kuona umuhimu wa Watanzania kupenda vya kwao.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/07/jkt-yajipanga-kufundisha-teknolojia-za.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa