Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini (JKT) Meja Jenerali Martin Busungu ameahidi kuwa Jeshi hilo litajenga Majengo ya kudumu katika Uwanja wa Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Nanenane Kanda ya Ziwa Mashariki wa Nyakabindi Bariadi Mkoani Simiyu, ili kuendelea kutoa elimu ya teknolojia mbalimbali za kilimo na ufugaji kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.
Meja Jenerali Busungu ameyasema hayo wakati alipotembelea eneo la JKT lililopo Uwanja wa Nanenane Nyakabindi kwa lengo la kujionea maandalizi hayo yanayofanywa na Jeshi la Kujenga Taifa.
Busungu amesema baada ya Nanenane wataanza ujenzi wa majengo ya kudumu ili wakulima, wafugaji na wavuvi wanufaike na teknolojia ya kilimo kwa muda wote.
“Mkuu wa mkoa ametupa mkakati wao kuwa kila baada ya miezi mitatu kutakuwa na maonesho katika uwanja huu, tunaahidi kujenga majengo ya kudumu hapa na maonesho yajayo miezi mitatu inayofuata wananchi watarajie kupata vitu vizuri kutoka JKT, maana JKT ni kisima cha kila kitu” alisema Meja Jenerali Busungu.
“ Katika maonesho haya watarajie kuona teknolojia mbalimbali za kilimo, ufugaji, uvuvi pia watarajie kuona bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na JKT zikiwemo bidhaa za kilimo, viwanda na kwa ndugu zangu Wanyantuzu wataona mbuzi na kondoo wa maziwa na wataona kuwa si ng’ombe tu wanaotoa maziwa” alisisitiza Meja Jenerali Busungu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameishukuru JKT kwa kazi kubwa ya maandalizi ya Maonesho ya Nanenane waliyoifanya, huku akibainisha kuwa uwepo wa JKT utasaidia kuwabaadilisha vijana wa Simiyu kwa kuwa watapata fursa ya kujifunza teknolojia mbalimbali.
“ Tunawashukuru sana JKT kwa kutuamini na tunajua kuwepo JKT kutasadia kuwabadilisha vijana wa hapa kwa kuwa kuna vijana wanamaliza darasa la saba au kidato cha nne hawana pa kushika na sisi tuna vikundi vingi vya vijana , tuko tayari kuleta vikundi vyetu vya vijana kuja kujifunza hapa” alisisitiza Mtaka.
Naye Mbunge wa Itilima amesema maonesho hayo yatawasaidia wananchi kupata elimu itakayowawezesha kufanya uzalishaji wenye tija ikiwemo ufugaji wa kisasa na kilimo bora.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/07/jkt-yaahidi-kujenga-majengo-ya-kudumu.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa