Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Balozi Dkt. Benson Bana ameiomba Wizara ya Fedha na Mipango kuwezesha ujenzi wa mabweni kwa wanafunzi takribani 500 wanaotarajiwa kudahiliwa mwezi Machi, 2020 katika Kampasi ya Kanda ya Ziwa ya Chuo hicho Mkoani Simiyu, ili kuwaondolea adha ya kupanga mitaani.
Dkt. Bana ametoa ombi hilo kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.Ashatu Kijaji alipofanya ziara Novemba 21, 2019 kuona maendeleo ya ujenzi wa kampasi hiyo kijiji cha Sapiwi wilayani Bariadi Mkoani Simiyu.
Dkt. Bana amesema kutokana na ongezeko la wanafunzi wanaoomba udahili wa masomo, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), kimeanzisha Kampasi ya Kanda ya Ziwa iliyopo Kijiji cha Sapiwi wilayani Bariadi Simiyu, ambapo mwezi Machi 2020 wanafunzi takribani 1000 wanatarajiwa kuanza masomo.
“Ili tuweze kufikia malengo yetu tunaomba mabweni ya kuhimili angalau wanafunzi 500 tu, Mhe. Naibu Waziri tunaomba kuwezeshwa kujenga mabweni haya mengine utuachie tutafanya, tusipofanikiwa hili Mhe. Naibu Waziri, juhudi za Mhe. Mkuu wa Mkoa na viongozi wenzake zinaweza kuishai mahali ambapo si pazuri,” alisema Dkt. Bana.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.Ashatu Kijaji amesema Serikali inatambua juhudi za Mkoa wa Simiyu katika elimu na kuahidi kujenga mabweni yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 500 kama alivyoomba Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo, ili wanafunzi watakaodahiliwa wapate malazi hususani wanafunzi wa kike.
“Hizi changamoto mlizozitaja na hasa hili la mabweni kwa ajili ya watoto wetu linafanyiwa kazi kwa haraka na ujenzi wa mabweni ya watoto 500 mpaka tutakapofika mwezi Machi inawezekana,” alisema Dkt. Kijaji.
Naye Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameushukuru uongozi wa Chuo cha IFM kwa uamuzi wa kujenga Kampasi mpya Simiyu na kuamua kuifungua mwaka 2020 ambapo amesema kuwepo kwa chuo hicho kutachangia kuongeza mwamko wa elimu katika mkoa wa Simiyu, huku akiwaalika wawekezaji kuwekeza katika huduma mbalimbali katika kampasi hiyo.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Prof.Tadeo Satta amewashukuru viongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa namna walivyowezesha kupata eneo la ujenzi lenye ukubwa wa ekari 30 ambalo lilitolewa bure na pia walivyosaidia katika hatua ya ujenzi ambapo wametoa wataalam kusaidia kusimamia ujenzi na kupelekea ujenzi kwenda kwa kasi.
Ameongeza kuwa majengo yanayotarajiwa kujengwa katika kampasi ya Simiyu ni jengo la utawala, maktaba, madarasa, maabara ya kompyuta, hosteli za wanafunzi, nyumba za wafanya kazi, kafteria na holi kwa ajili ya mikutano; ambapo kwa awamu ya kwanza ujenzi ulianza mwezi Julai 2019 mpaka sasa jengo la utawala lenye ghorofa moja limefikia asilimia 62 na madarasa yamefikia asilimia 92.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/11/dkt-bana-aomba-wizara-ya-fedha.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa