Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amewaomba wadau wa afya waliopo mkoani Simiyu kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya kwa kutenga bajeti kwa ajili ya kuchangia ununuzi wa vitendea kazi na kujenga miundombinu ya afya.
Kiswaga amevitaja vitendea kazi hivyo kuwa ni pamoja na magari ya kubebea wagonjwa (ambulance), vifaa vya kwenye vituo vya afya ,zahanati na hospitali ili huduma ziendelee kutolewa kwa ufanisi mkubwa.
Ameyasema hayo katika kikao cha wadau wa afya kilichofanyika Mjini Bariadi wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kwenye kikao cha wadau wa afya kilichofanyika Julai 11 na Julai 12, 2019 kwenye ukumbi wa kanisa Katoliki mjini Bariadi.
Aidha ameongeza kuwa kuna kila sababu ya mashirika hayo kuongeza majengo na magari ili huduma za afya zizidi kuimarika mkoani hapo.
Pamoja na hayo amesema kuwa kama mkoa watahakikisha wanatoa ushirikiano wa kutosha kwa wadau wa afya mkoani hapo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
"kila shirika lililopo mkoani hapa linafanya kazi nzuri endeleeni kuzidisha juhudi hizo bado tuna upungufu wa vitendea kazi , tunaomba muendelee kutafuta fedha huko ili kuhakikisha kwamba vitendea kazi kama magari, magari ya kubebea wagonjwa lakini pia majengo bado ni changamoto pamoja na kazi kubwa nzuri ambazo mmezifanya tunaombeni muendelee kuweka bajeti hizo "alisema Kiswaga na kuongeza kuwa:
“kama mkoa tutahakikisha mashirika haya yanatekeleza majukumu yake bila wasiwasi wowote , watendaji kuanzia ngazi za chini sitegemei kusikia shirika limeshindwa kutekeleza shughuli zake eti kisa mtendaji kakwamisha , watendaji kuanzia ngazi ya chini hakikisheni mnatoa ushirikiano wa kutosha ili mashirika haya yatekeleze majukumu yake”aliongeza Kiswaga
Kwa upande wake Mwenyekiti wa wadau wa afya mkoani hapa Dkt Amiri Batenga ambaye ni mwakilishi wa shirika la umoja wa kimataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani UNFPA mkoa wa Simiyu amesema kuwa wameendelea kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya lengo likiwa kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto wachanga.
Aidha, Dkt. Batenga ameongeza kuwa wameshatumia kiasi cha bilioni tano na nusu kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majengo ,vifaa pamoja na magari mkoani Simiyu huku akiomba Serikali kuendele kusimamia na kuhakikisha vituo na vifaa hivyo vinafanya kazi iliyokusudiwa na wananchi waone haja ya kutumia vituo hivyo maana vimejwngwa kwa ajili yao.
“kujenga vituo vya afya ,kuweka vifaa na kufundisha watumishi ni jambo jingine vituo hivi vinatakiwa vitumike kina mama wajawazito wasipotumia hivi vituo yale malengo hayawezi fikiwa …pale tumejenga vituo 38 nasasa hivi tumeongeza vingine viwili ili kufikia malengo lazima mama aje pale tukiunganisha nguvu ya pamoja kina mama wakafika kwenye vituo vya afya vifo vitaisha kabisa” alisema Batenga
Mkoa wa Simiyu una zaidi ya mashirika 17 yanayofanya kazi bega kwa bega na mkoa yakiwa na lengo la kuunga mkono juhudi za serikali katika sekta mbalimbali ikiwemo afya na elimu.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/07/dc-bariadi-wadau-wa-afya-endeleeni.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa