Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista wa Sabato, Jimbo Kuu la Kaskazini mwa Tanzania, Dkt.Mch. Godwin Lekundayo ameongoza viongozi na mamia ya waumini wa kanisa hilo katika ibada maalum ya kumshukuru Mungu kwa kulivusha Taifa katika Janga la Corona pamoja na kusaidia Uchaguzi Mkuu kumalizika kwa amani hapa nchini.
Ibada hiyo imefanyika katika Kanisa la Waadventista Wasabato Bariadi la Mtaa wa Ntuzu lililopo Bariadi mjini ambapo Waumini wa kanisa hilo pamoja na wengine kutoka mkoa wa Mwanza na Mara wamewakilisha waumini wengine hapa nchini, ambapo ibada hiyo imehudhuriwa pia na viogozi wa Chama na Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka.
“Nilikuwa naangalia takwimu za hali ya janga la Corona ilivyo duniani leo asubuhi (Desemba 05, 2020) hadi sasa zinaonesha watu 66,281,000 wamepatwa na Corona, waliokufa mpaka sasa 1,525,294 ikiwa ulikuwa umechukulia kiurahisi, hizi takwimu zikuamshe kwamba Mungu ametupendelea sana Tanzania tunamshukuru sana Mungu kwa niaba ya wenzetu,” alisema Dkt. Lekundayo.
Awali akitoa mahubiri kabla ya maombi hayo pamoja na kuwasihi waumini kumshukuru Mungu kuwapitisha katika janga la Corona, Askofu Lekundayo pia ametoa wito kwa waumini kuendelea kumshukuru Mungu pia kwa namna ambavyo amelipitisha Taifa katika Uchaguzi Mkuu, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya jambo ambalo litabaki kumbukumbu yao juu ya neema ya Mungu katika masuala hayo.
Akitoa salamu za Serikali kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amesema Tanzania kupitishwa katika Janga la Corona haikuwa bahati bali ni neema ya Mungu, hivyo akawashukuru viongozi wa Dini kwa kuliombea Taifa kwa juhudi na Mungu akajibu.
Aidha, Kiswaga amesema Serikali inaendelea kuheshimu mchango wa kanisa na itaendelea kushirikiana nalo katika majukumu yake ya kitume na kimaendeleo, huku akitoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa na viongozi wake ili waweze kufanya kazi kwa manufaa na ustawi wa Watanzania.
“Katika neno la Mungu kuna habari ya wale wakoma kumi ambao waliponywa na Bwana Yesu lakini aliyerudi kushukuru ni mmoja tu, ninaamini maombi haya ya shukrani yaendelea kuiponya nchi yetu na majanga ambayo yanaonekana kwa macho na ambayo hayaonekani,” alisema Kiswaga.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Mhe. Samweli Kiboye amesema kuna baadhi ya watu waliobeza Mhe Rais alivyotangaza kumtanguliza Mungu kwa kutangaza siku tatu za kuliombea Taifa ili aliponye Taifa na Janga la Corona lakini baada ya kuona matokeo ya maombi naamini wameona kuwa maamuzi yake yalikuwa sahihi.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2020/12/askofu-lekundayo-aongoza-maombi.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa