Shirika lisilo la kiserikali la AMREF limetoa msaada wa gari la kubebea wagonjwa lenye thamani ya shilingi milioni 150 katika Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu ambalo
litatumika kuharakisha rufaa za wagonjwa hususani wakinamama wajawazito na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi Mkoani humo. .
Akikabidhi gari hilo kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka,Meneja wa AMREF wa program wa Afya ya mama na Mtoto Tanzania Dr.Sarafina Mkuwa amesema kuwa Shirika hilo kupitia Mradi wa Uzazi Uzima umetambua umuhimu wa kutatua changamoto katika sekta ya afya na kutoa gari hilo ili kunusuru vifo vya akinamama na watoto Mkoani Simiyu.
“Hii ‘ambulance’itasaidia wagonjwa watakaohitaji huduma za rufaa kwa haraka, Mkuu wa Mkoa nakukabidhi ambulance hii ili iweze kuusaidia mkoa katika kuhakikisha kwamba wakina mama wa Mkoa wa Simiyu wanajifungua salama na wanapata huduma zote za rufaa kwa haraka” alisisitiza Dkt. Mkuwa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameishukuru AMREF kwa kutoa gari hilo ambapo amesema msaada huo umejibu hoja ya Mkoa huo waliyokubaliana na wadau wa afya kuwa fedha za wadau hao zinapaswa kujibu mahitaji ya wananchi katika sekta ya afya, ikiwa ni pamoja na vitendea kazi kama magari na kujenga miundombinu ya afya badala ya kuzielekeza zaidi kwenye semina.
Aidha, amesema gari hilo litakuwa msaada mkubwa kwa Hospitali Teule ya mkoa ambayo hapo awali ilikuwa ikiilazimu kuazima magari kutoka katika hospitali na vituo vingine vya afya pale huduma za haraka zinapohitajika kwa ajili ya kuwasafirisha wagonjwa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
“Tunawashukuru sana AMREF kwa msaada huu, gari hili litatusaidia sana kwenye hospitali yetu maana walikuwa wakipata dharura ‘ambulance’ inaitwa kutoka kwenye maeneo mengine, jana Mhe.Esther Midimu Mbunge wa Viti Maalum (CCM) aliuliza ni lini Hospitali ya Mkoa wa Simiyu itapata gari la wagonjwa leo AMREF wamejibu swali lake” alisema Mtaka
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa huyo amewahakikishia viongozi wa AMREF kuwa Serikali mkoani humo itaendelea kushirikiana nao katika masuala mbalimbali ya kuboresha huduma za afya na kutatua changamoto za sekta ya Afya kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Mkoa,Dkt. Fredrick Mlekwa amesema wanalishukuru shirika la Amref kwa msaada huo kwani hapo awali walikuwa wakipata shida kuazima gari hilo katika wilaya zingine za Mkoa na akaahidi kuwa Hopsitali hiyo italitunza gari hilo na kulitumia kwa lengo lililokusudiwa..
Mwisho
KUPATA PICHA ZAIDI JUU YA HAFLA YA MAKABIDHIANO YA GARI HILI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/05/amref-watoa-gari-ya-wagonjwa-hospitali.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa