Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Mary Mwanjelwa ametoa wito kwa wanafunzi wa kidato cha nne mkoani Simiyu ambao walipata ufaulu hafifu katika mtihani wa utimilifu (mock) walioko kambi ya kitaaluma ,kutumia fursa hiyo kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao.
Dkt Mwanjelwa ametoa wito huo alipowatembelea wanafunzi hao katika kambi ya kitaaluma iliyopo chuo cha ualimu Bariadi mkoani hapa na kuwasisitiza walimu mbali na kuwafundisha masomo ya darasani pia wawafundishe namna ya kukabiliana na maisha baada ya kumaliza masomo ili ambao hawatabahatika kuendelea na masomo ya juu waweze kujiajri na kuajiri wengine.
Katika hatua nyingine Mwanjelwa amewataka wanafunzi kuitumia fursa ya uwepo wao kambini kufanya kile kilichowapeleka, watumie muda mwingi kujifunza na wajiepusha na mahusiano ya kimapenzi ambayo yatawasababishia kushindwa kutimiza malengo yao ya baadaye.
“Maisha bila malengo sio maisha nini matarajio yako baada ya kusoma na endepo hutafaulu ujue namna ya kujiajiri, tumieni fursa ya kuwa hapa kuhakikisha mnasoma kwa bidii ishike sana elimu MUNGU hatakuacha, maisha lazima myatafute ,myatolee jasho, ” alisema Mwajelwa
“Wanafunzi wa kike jitunzeni lindeni utu wenu asitokee mtu akawadanganya mkashindwa kufikia ndoto zenu ninyi ni wa thamani kubwa kumbukeni mbali na mimba kuna magonjwa, ” aliongeza Dkt Mwanjelwa.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesema kama mkoa wataendelea kusimamia fedha zote zinazotolewa na serikali ya awamu ya tano za elimu bila malipo ili ziweze kuleta matokeo chanya .
“Tunatamani kuona elimu bure inayotolewa na serikali inazaa matunda tutapambana kuhakikisha vituo vya kutolea elimu vinakuwa na mazingira bora na kama mlivyomuahidi kwa ziro hakuna na iwe hivyo, ”alisema Sagini
Awali baadhi ya wanafunzi waliopo kambini hapo wamemshukuru mkuu wa mkoa huo kwa kuanzisha kambi za kitaaluma ambazo wamesema zimewawezesha kuwa na uwelewa wa masomo mbalimbali kupitia walimu mahiri hatua iliyowatoa kwenye daraja sifuri mpaka daraja la 111 kupitia mitihani mbalimbali wanayopewa kambini hapo..
“Nilikuja kambini hapa nikiwa na division ziro tulivyofanya mtihani wa mock ufaulu uliongezaka na nikikapata division 111 awali nilikuwa sijui kuandika essay sasa hivi najua na nina uwezo wa kuandika barua ya kuomba kazi ninachokuhakikishia mhe,pamoja na mkoa chini ya mkuu wetu wa mkoa hatutawaangusha alisema ” Pendo Aguda kutoka shule ya sekondari Old Maswa.
Akiwa kambini hapo Dkt. Mwanjelwa amekabidhi kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Itilima Mhe.Njalu Silanga kilo elfu moja za unga wa mahindi, kilo mia tano za mchele na mafuta ndoo ishirini kwa ajili wanafunzi walioko kambini.
MWISHO
KUPTA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/10/dkt-mwanjelwa-atoa-neno-kambi-za.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa