Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa minane inayolima pamba kwa wingi nchini ikiongozwa na mkoa wa Simiyu kusimamia kikamilifu uzalishaji wa zao hilo katika msimu huu na kuhakikisha wakulima wanapewa elimu stahiki itakayowawezesha kuongeza tija katika kilimo cha zao hilo.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo katika mkutano uliomwezesha kuwasiliana moja kwa moja kwa njia ya video (Video conference) na wakuu wa mikoa ya Simiyu, Mara, Shinyanga, Geita, Kagera, Mwanza, Tabora na Singida na kusema kuwa msimu huu hatarajii kuona changamoto zilizoshusha kiwango cha uzalishaji katika msimu uliopita zinajirudia huku akimwagiza mkurugenzi mkuu wa bodi ya pamba nchini kuhakikisha dawa za kuua wadudu zinawafikia wakulima kwa wakati.
“ Mwaka huu lengo letu ni kuzalisha tani laki sita, ninaamini hili linawezekana endapo ninyi waheshimiwa wakuu wa mikoa mtalisimamia jambo hili kikamilifu, nendeni mkahakikishe maafisa ugani pamoja maafisa ushirika wanatoka ofisini na kuwatembelea wakulima katika maeneo yao na kuwaelimisha kuhusu namna ya kupata mitaji pamoja na uwezekano wa kupata soko la uhakika baada ya mavuno”.
“Tukiwa bado katika ngazi ya mkoa, pia hakikisheni mnawasimamia Makatibu tawala wanaoshughulikia kilimo pamoja mrajisi wafuatilie mara kwa mara kujiridhisha kama agizo hili linatekelezwa kwa vitendo”, alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha Waziri Mkuu Majaliwa ameagiza mikoa ipitie upya utaratibu unaotumika hivi sasa unaoruhusu fedha yote inayokusanywa kupelekwa kwenye miradi ya maendeleo na badala yake uanzishwe utaratibu mpya utakaoruhusu sehemu ya makusanyo hayo kutumika kuboresha kilimo cha pamba.
Akijibu swali laWaziri Mkuu Majaliwa kuhusu utaratibu unaoweza kumsaidia mkulima kuondokana na dhana ya utegemezi wa mikopo, Mkuu wa mkoa wa Simiyu mkoa ambao ndiye mzalishaji mkuu wa pamba nchini kwa 55% Anthony Mtaka amesema, njia pekee itakayowasidia wakulima kuondokana na hali hiyo ni bodi ya pamba kutochukua sehemu ya mapato ya shilingi 100 kwa kila kilo kama ambavyo imekuwa ikifanya badala yake fedha hizo zibaki kwenye AMCOS kama njia ya kuimarisha kilimo cha zao hilo.
“ Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa upande wetu Simiyu msimu huu pekee tunatarajia kuvuna kilo milioni 240, na kama bodi ya pamba watachukua kiasi cha shilingi 100 kwa kila kilo kama ambavyo wamekuwa wakifanya maana yake watachukua shilingi bilioni 24, ambazo kama zikibaki kwenye AMCOS si haba, ndio maana tunasisitiza ipo haja ya kuutazama upya mfumo huu na endapo sote tutaafiki kuufanyia mabadiliko, Simiyu tupo tayari kuwa wa kwanza kulitekeleza na tutaanza na wilaya mojawapo tuone kama una tija”, aliongeza Mhe Mtaka.
Huu ni mkutano wa kwanza wa aina hii kati ya waziri mkuu na wakuu wa mikoa ambapo ameiagiza kampuni ya simu TTCL kuhakikisha mifumo yote inayoruhusu mawasiliano ya moja kwa moja kwa njia ya video inafanya kazi katika ofisi zote za wakuu wa mikoa nchini ambapo hivi karibuni kwa mara nyingine anatarajiwa kufanya mkutano kama huu na wakuu wa mikoa 4 inayolima chai kwa wingi nchini ikiwemo Tanga, Iringa, Njombe na Mbeya.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa