Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Geita wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi. Robert Gabriel kwa ubunifu waliofanya wa kufanya Maonesho ya Kipekee ya Tekonolojia bora ya dhahabu hapa nchini.
Mtaka ameyasema hayo mara baada ya kuzungumza na viongozi wa Mkoa wa Geita na kutembelea mabanda ya maonesho katika Maonesho ya Teknolojia ya Dhahabu yanayofanyika Uwanja wa CCM Kalangalala Mjini Geita kuanzia Septemba 24, 2018.
Amesema Watanzania wengi wamekuwa wakienda kushiriki maonesho ya dhahabu katika mataifa mbalimbali barani Afrika na nje ya bara la Afrika lakini kupitia maonesho haya Watanzania wameanza kujionea teknolojia mbalimbali za uchimbaji wa madini hapa nchini.
“ Ninawapongeza sana viongozi wa Geita kwa kuandaa maonesho haya ya kipekee hapa nchini, tumekuwa na shughuli nyingi sana za uchimbaji madini lakini sisi sote ni mashahidi shughuli hizi tumekuwa tukiziona wakati wa Mei Mosi kupitia kile chama kinachohusisha watu wanaofanya kazi za madini, hatujapata jambo linaloonesha shughuli za migodini na mazao yanayotokana na migodi kama dhahabu” alisema Mtaka.
Ameongeza kuwa ubunifu huo uliofanywa na Viongozi wa Mkoa wa Geita hasa wa kuyapa maonesho haya jina la Kiswahili ya “Maonesho ya Dhahabu” ambalo linasadifu shughuli zinazofanyika katika mkoa huo ambao ni mzalishaji mkubwa wa dhahabu, utachangia kuongeza watalii na wageni wengi watakaokuja hapa nchini kupitia maonesho hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi. Robert Gabriel ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kushuhudia maonesho hayo ili kujionea teknolojia za uchimbaji madini, kupata huduma za kifedha katika taasisi za kifedha, kupata huduma na elimu juu ya utatuzi wa changamoto za kibiashara hususani upatikanaji wa mitaji na changamoto za uchimbaji katika kliniki ya biashara.
Aidha, Mhandisi. Gabriel amesema maendeleo katika mkoa wa Geita hayaepukiki kutokana na sekta ya madini kuwa na mchango mkubwa katika uchumi ambapo amebainisha kuwa kupitia uchimbaji dhahabu mkoa unapata ushuru, fedha za msaada kwa jamii (Corporate Social Responsibility) kutoka kwenye makampuni yanajihusisha na uchimbaji madini zilizosaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Mhe. Leonald Bugomola amesema maonesho ya dhahabu mwaka 2019 yataanza mapema na Halmashauri yake kama mwenyeji wa maonyesho hayo imejipanga kutafuta eneo kubwa zaidi ekari 100 , kwa kuwa mpango wa mkoa ni kuwa na maonesho yenye hadhi ya Kimataifa yatakoshirikisha washiriki wengi ikilinganishwa na mwaka huu.
Nao baadhi ya wachimbaji wadogo wameshukuru uanzishwaji wa maonesho hayo ambayo yatasaidia kupata utaalamu juu teknolojia mbalimbali zinazotumika kuchimba madini na kupata elimu ya namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika sekta ya madini kutokana na wadau mbalimbali kukutanishwa pamoja na kujadiliana kuhusu maendeleo ya sekta ya madini.
Maonesho ya Tekonolojia Bora Dhahabu mkoani Geita yameanza Septemba 24, 2018 na yanatarajiwa kuhitimishwa Septemba 30, 2018 yakiwa na Kauli Mbiu: TEKNOLIJIA BORA YA UZALISHAJI WA DHAHABU KWA MAENDELEO YA KIJAMII NA UCHUMI WA VIWANDA”
MWISHO.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa