Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kinatarajia kujenga Tawi jipya katika Kata ya Sapiwi Tarafa ya Dutwa wilayani Bariadi Mkoani Simiyu.
Viongozi wa chuo hicho wakiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Tadeo Andrew Satta wametembelea eneo hilo leo Machi 26, 2019 na baadaye kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa Mkoa wa Simiyu ambapo wamekubaliana kushirikiana katika hatua zote kuanzia upimaji wa eneo mpaka ujenzi wa majengo ya chuo.
Akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu, Makamu Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Prof. Tadeo Andrew Satta amewashukuru viongozi hao kwa kutoa eneo la ekari ishirini bure akaahidi kushirikiana na Serikali mkoani hapa kuhakikisha tawi hilo linajengwa mkoani Simiyu ili kusogeza karibu huduma kwa wananchi wa Simiyu.
Awali akizungumza na viongozi hao Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema Serikali mkoani humo iko tayari kushirikiana na viongozi wa Chuo hicho kwa kutoa wataalam watakaosaidia katika Usimamizi wa upimaji na akashauri ujenzi wa majengo ya chuo hicho ufanyike kwa kutumia mfumo wa ‘Force Account’ ili kupunguza gharama.
Amesema mfumo huu utapunguza gharama kwa kuwa hautumii wakandarasi badala yake ujenzi utafanywa na mafundi wa kawaida wakisimamiwa na wahandisi wa ujenzi Mkoa na Halmashauri mkoani Simiyu huku vifaa vyote vya ujenzi vikinunuliwa kwa pamoja na chuo hicho.
Aidha, amemhakikishia upatikanaji wa wanafunzi kwa kuwa hadi sasa Mkoa wa Simiyu bado una Vyuo vichache vya elimu ya juu, huku akibainisha kuwa tayari Serikali mkoani hapa imeshatoa ardhi bure kwa ajili ujenzi wa Matawi ya Vyuo mbalimbali vya elimu ya juu ikiwemo Chuo cha Mipango, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo cha Mahakama.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesema wanaendelea kushawishi Taasisi nyingi za Elimu ya Juu kujenga matawi yake Mkoani hapa, ili kutoa nafasi kwa Wanasimiyu kupata elimu ya juu itakayochangia kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kijamii.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/03/ifm-kujenga-tawi-jipya-simiyu.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa