Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Fabian Manoza amesema Matumizi ya Mbegu bora na Kilimo cha Mkataba ni suluhu ya wakulima wa pamba inayoweza kuwasaidia kuongeza uzalishaji.
Manoza ameyasema hayo wakati akitoa taarifa ya Wilaya ya Meatu kuhusu kilimo cha Pamba kwa Wakuu wa Mikoa nane ya Kanda ya Magharibi inayolima pamba waliotembelea eneo hilo kutoka Simiyu,Shinyanga, Geita, Mwanza, Kagera, Kigoma, Singida na Tabora katika ziara yao kuona mashamba ya uzalishaji wa mbegu bora ya pamba(UKM08) katika kata ya Mwabusalu wilayani Meatu.
Amesema kupitia kilimo cha mkataba wananchi watakuwa na uhakika wa kupata pembejeo bora za kilimo zikiwemo mbegu bora, mbolea na viuadudu kutoka kwa watu au makampuni yatakayoweka mikataba nao.
“Tunatarajia kuongeza uzalishaji ilikupata kata nyingi zaidi, tumewasisitiza wananchi kuwa kilimo hiki cha mbegubora lazima kiendane na kilimo cha mikataba, wale wanaohitaji kununua pamba lazima waingie mikataba na wakulima ili wapate faida walizokuwa hawazipati;baadhi yao wamekuwa wakihangaika hawana uwezo wa kununua mbegu, viuadudu na kuhudumia mashamba, lakini wakiingia mikataba hao watakaonunua pamba watatoa huduma zote hizo kwa wakulima” alisema.
Ameongeza kuwa pamoja na kilimo cha mkataba na matumizi ya mbegu bora ili kuboresha uzalishaji wa pamba Wataalam wa Kilimo wanapaswa kuwapa wakulima huduma zote muhimu zaugani ili wazingatie taratibu zote za kuandaa mashamba, upandajina utunzaji wa pamba.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. MejaJenerali Ezekiel Kyunga ameitaka Bodi ya Pamba nchini kuboresha utaratibu wa kilimo cha mkataba ili kiweze kuwanufaisha wakulima badala ya kuwakatisha tamaa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora,Mhe.Aggrey Mwanri amesema ni vema Bodi ya Pamba ikaweka utaratibu utakaowawezesha wakulima kupata mbolea na zana bora za kilimo kwa mkopo ambao watarejesha baada ya mavuno.
Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba,Marco Mtunga amesema wakulima wa pamba kwa miaka ya nyuma wamekuwa wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mbegu bora na kutopanda kwa kuzingatia mistari, hivyo katika msimu wa mwaka 2017 jumla ya tani 8000 za mbegu bora zitazalishwa kwa ajili ya kusambaza kwa wakulima najitihada zinaendelea kufanywa kupitia kilimo cha mkataba kuhamasisisha wakulima kulima kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu.
Aidha, Mtunga amesema ili kuongezauzalishaji wa pamba wakulima wahamasishwe kulima kilimo cha mkataba naili kilimo cha mkataba kiwe na tija kwao Bodi hiyo inaendelea kutimiza wajibu wake kusimamia masharti yaliyowekwa katika utekelezaji wa mikataba hiyo kati ya wachambuzi na wakulima wa pamba.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida,Mhe.Dkt.Rehema Nchimbi amesisitiza kuwepo kwa mikakati ya kilimo cha umwagiliaji katika zao la pamba ikiwepo uchimbaji wa mabwawa makubwa yatakayowasaidia wakulima wakati wote badala ya kutegemea mvua tu.
Naye Bw.Charles Thobias Mkulima wa kata ya Mwabusalu ambaye ametumia mbegu bora ya pamba ya (UKM08) amesema mbegu hiyo imekuwa mkombozi kwa wakulima kwa kuwa kulingana na mazao yalivyo sasa shambani, mavuno yataongezeka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na msimu uliopita.
Utekelezaji wa Mpango wa uzalishaji wa Mbegu bora katika kata ya Mwabusalu Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu umehusisha jumla ya wakulima 1,709 katika vijiji vinne ambao kwa pamoja wameweza kulima jumla ya ekari 6,506 na unafadhiliwa na Programu ya Kuendele za Kilimo cha Pamba chini ya usimamizi wa Bodi ya Pamba.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa